WANASIASA wanaowania urais mwaka wa 2027 wanakabiliwa na changamoto kubwa katika ngome zao, huku wapinzani katika maeneo wanakotoka wakitishia kuvuruga ushawishi wao kabla hata hawajaanza kampeni za kitaifa.
Kutoka Mlima Kenya, Ukambani, Magharibi, Gusii hadi Bonde la Ufa, viongozi wanaotaka kuingia Ikulu wanapambana na wanasiasa wenzao wanaotaka kuwa na usemi katika maamuzi ya kisiasa ya maeneo hayo.
Hali hii inazua swali kuu: Je, wanasiasa wanaweza kujenga miungano ya kitaifa ya kumng’oa Rais William Ruto bila kwanza kuhakikisha kuwa wanaungwa mkono kikamilifu katika ngome zao za kisiasa?
Kwa Naibu wa Rais wa zamani Rigathi Gachagua, mtihani mgumu ni kudumisha ushawishi wake Mlima Kenya, eneo ambalo kura zake zilimsaidia Rais Ruto kushinda uchaguzi wa 2022.
Kiongozi huyo wa chama cha DCP anasuka muungano wa upinzani unaohusisha Wiper ya Kalonzo Musyoka na chama cha Linda Mwananchi kinachoongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna.
Hata hivyo, mpango huo unakabiliwa na upinzani kutoka kwa wanasiasa wa Mlima Kenya ambao hawataki Gachagua ajitawaze kuwa kiongozi wao pekee.
Miongoni mwao ni Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, ambaye amekuwa akijenga upya ushawishi wake kupitia chama cha People's Party of Kenya (PPK) na kushirikiana na viongozi kama Martha Karua wa chama cha People's Liberation Party (PLP) na Fred Matiang’i wa Jubilee.
Viongozi wengine wenye misimamo yao ni Justin Muturi wa Democratic Party na Jimi Wanjigi wa Safina.