TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na wabunge wamezozana kuhusu mamlaka ya kuidhinisha kanuni mpya zinazoweka viwango vya fedha ambazo wagombeaji wataruhusiwa kutumia katika kampeni za uchaguzi mkuu wa 2027.
Mzozo huo ulijitokeza katika kikao kati ya IEBC na Kamati ya Bunge la Kitaifa, huku kila upande ukisisitiza kuwa una mamlaka ya kisheria kuhusu kanuni hizo.
Kamati hiyo, inayoongozwa na Mbunge wa Ainabkoi, Samuel Chepkong’a, inasema kanuni hizo zinapaswa kuwasilishwa bungeni ili wabunge wazichunguze, wazirekebishe au kuzikataa kabla ya kuanza kutekelezwa.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Ethekon, alikataa msimamo huo, akisema sheria haihitaji kanuni hizo kuidhinishwa na Bunge.
“Mnazichapisha kwenye gazeti la serikali lakini hamkuzileta bungeni kwa ukaguzi. Kila jambo lenye nguvu ya sheria lazima lipitie bungeni,” alisema Bw Chepkong’a, akirejelea Ibara ya 94(5) ya Katiba.
Lakini Bw Ethekon alimjibu kuwa suala hilo tayari lilitatuliwa na mahakama, ambayo iliamua kuwa kanuni hizo zinaweza kuchapishwa bila kuidhinishwa na Bunge, mradi wananchi washirikishwe.
“Sheria haihitaji idhini ya Bunge. Kanuni hizo huanza kutekelezwa zenyewe,” alisema.
Kanuni hizo zilichapishwa katika gazeti la serikali Agosti 7, 2026, zikiwa na lengo la kudhibiti matumizi ya fedha katika uchaguzi na kuzuia wagombeaji matajiri kuwazidi wengine kwa kutumia fedha nyingi.
Kwa mfano, mgombeaji wa urais ataruhusiwa kutumia hadi Sh6.11 bilioni katika kipindi cha kampeni, huku wagombeaji wa nyadhifa za kaunti wakiwa na viwango tofauti kulingana na…