RAIS Mstaafu Uhuru Kenyatta amewataka viongozi wa upinzani kuweka kando tamaa zao za kibinafsi za kuwania urais na kuungana nyuma ya mgombea mmoja, akisema Wakenya tayari wameamua kumwondoa Rais William Ruto mamlakani katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2027.
Bw Uhuru alisema changamoto kubwa inayokabili upinzani si ukosefu wa wananchi wanaotaka mabadiliko, bali viongozi wake kukosa kukubaliana kuhusu mwelekeo mmoja wa kisiasa.
Alionya kuwa ushindani wa viongozi kutaka kuwania urais unaweza kuvuruga juhudi za kuunda muungano ulio na msimamo mmoja dhidi ya utawala wa Kenya Kwanza.
Alitaja kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, akiwakumbusha kuwa kiti cha urais kinaweza kushikiliwa na mtu mmoja pekee kwa wakati mmoja.
“Tunapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu mustakabali wa nchi yetu, wala si yaliyopita. Ninawaambia ndugu zangu Kalonzo, Rigathi Gachagua na Eugene kwamba mtu mmoja pekee ndiye anaweza kukalia kiti hicho kwa wakati mmoja,” alisema.
Alikuwa akizungumza jana wakati wa ibada ya mazishi ya binamu yake Beatrice Wambui Muturi katika Kanisa la PCEA Nairobi West, Lang’ata, Nairobi.
Bw Kenyatta alisema mazungumzo yake na Wakenya wa kawaida, hata anapokwenda “kununua uji”, yamemshawishi kuwa wananchi wanataka mabadiliko ya uongozi.
Hata hivyo, alisema wanataka kwanza kuona viongozi wa upinzani wakimaliza tofauti zao.
“Ingawa nimestaafu, masikio yangu hayajafungwa. Ninazungumza na watu na kuwasikiliza.