WABUNGE wameanzisha hatua za kuimarisha vita dhidi ya wahalifu wanaoficha fedha zinazotokana na uhalifu kwa kuzibadilisha kuwa sarafu za kidijitali ili kuficha chanzo chake.
Pendekezo la kurekebisha sheria ya kukabiliana na ulanguzi wa fedha linalenga kupatia idara za uchunguzi mamlaka zaidi ya kufuatilia, kuzima na kutwaa mali ya kidijitali inayohusishwa na uhalifu.
Hatua hiyo inawalenga pia wanaojulikana kama ‘wash wash’ au ‘sharp boys’, ambao baadhi yao hutumia mifumo ya kifedha na teknolojia kuficha fedha zinazotokana na shughuli haramu.
Sarafu za kidijitali ni fedha zinazohamishwa kwa njia ya kielektroniki bila kutegemea mifumo ya kawaida ya benki.
Miamala yake hurekodiwa kupitia teknolojia ya blockchain, ambayo hutumika kuhifadhi na kuthibitisha taarifa za kuhamisha fedha.
Mnamo Jumanne, wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Haki na Masuala ya Kisheria waliunga mkono pendekezo la Shirika la Kufuatilia na Kurejesha Mali (ARA) la kurekebisha Sheria ya Mapato ya Uhalifu na Kupambana na Ulanguzi wa Fedha.
Marekebisho hayo yanapendekezwa kupitia mswada wa mwaka 2026 ambao kwa sasa unachunguzwa na kamati hiyo kabla ya kuwasilishwa kwa Spika wa Bunge kwa hatua zaidi.
ARA inataka ufafanuzi wa mali katika sheria hiyo upanuliwe kujumuisha sarafu za kidijitali na mali nyingine inayohifadhiwa kupitia teknolojia ya kisasa.
Kwa mujibu wa shirika hilo, hatua hiyo itatoa msingi wa kisheria kwa maafisa wa uchunguzi kutambua, kufuatilia, kuzima na kutwaa mali hiyo inapohusishwa na uhalifu.