RAIS William Ruto amemshambulia mtangulizi wake Uhuru Kenyatta, akimtaja kama dalali wa kisiasa anayepoteza muda kuwaunganisha viongozi wa upinzani badala ya kushughulikia changamoto zinazowakabili Wakenya.
Ruto alisema Uhuru ameachana wajibu wake kama kiongozi wa kitaifa na sasa anashughulika kutafuta mgombea mmoja wa upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Alikuwa akizungumza jana alipohitimisha ziara yake ya siku nne katika eneo la Gusii, iliyohusisha kaunti za Kisii na Nyamira.
“Nimesikia kuhusu huyo sponza, rafiki yangu. Je, hamumjui? Ameacha kuwa kiongozi wa kitaifa na sasa amekuwa dalali. Anajaribu kuunganisha huyu na yule. Namwambia aharakishe kazi yake ya udalali na atafute mtu anayemtafuta,” alisema Ruto.
Rais alidhihaki juhudi za upinzani kupata mgombea wa pamoja, akisema viongozi hao wamekuwa wakizunguka hoteli, nyumba za watu na mazishi kwa mwaka mmoja na nusu bila kufikia makubaliano.
Alisema ikiwa viongozi hao wanachukua muda mrefu kukubaliana kuhusu mgombea mmoja, itakuwa vigumu kwao kupanga masuala ya nchi yenye watu milioni 60.
“Wamekuwa kwa mwaka mmoja na nusu wakimtaja huyu au yule kuwa mgombea wao. Wanazunguka kutoka hoteli moja hadi nyingine na nyumba moja hadi nyingine. Ikiwa wanachukua muda wote huo kupata mgombea mmoja, watawezaje kupanga mambo ya watu milioni 60?” aliuliza.
Aliongeza kuwa yuko tayari kukabiliana na upinzani bila kujali iwapo utawasilisha mgombea mmoja, kumi au hata 1,000.