KIONGOZI wa Linda Mwananchi, Seneta Edwin Sifuna anatarajiwa kuanza ziara ya wiki mbili nchini Amerika ili kuwavutia wapigakura ughaibuni na kuchangisha fedha za kugharimia azma yake ya urais.
Seneta huyo wa Nairobi pamoja na wandani wake wanatarajiwa kuanza ziara hiyo Novemba 20, ambapo watakutana na Wakenya wanaoishi katika miji mbalimbali ya Amerika.
Miongoni mwa viongozi wakuu wa chama hicho wanaotarajiwa kuandamana naye ni mwenyekiti na Senata wa Vihiga Godfrey Osotsi, Mwekahazina Richard Onyonka na naibu kiongozi wa chama Faith Odhiambo.
Mkuu wa mawasiliano wa Linda Mwananchi Pauline Njoroge aliiambia Taifa Leo kuwa chama hicho kilikuwa kikikamilisha ratiba ya ziara kabla ya kuitangaza rasmi kwa umma.
“Kuna mambo mengi yanayohusika na tukikamilisha maandalizi, tutatangaza ratiba kamili pamoja na maelezo yote,” akasema.
Hata hivyo, ratiba iliyochapishwa katika mtandao wa chama hicho inaonyesha kuwa Bw Sifuna atazuru AllenTown kuanzia Novemba 20 hadi 22.
Kisha atasafiri hadi sehemu ya jiji kuu Washington (DMV) kati ya Novemba 23 na 24, Dallas mnamo Novemba 27 na 28, Houston mnamo Novemba 29 na 30, kabla ya kuhitimisha ziara yake kwa kutembelea Seattle na California kati ya Desemba 1 na 4.
Ziara hiyo inajiri miezi kadhaa baada ya Kiongozi wa DCP Rigathi Gachagua kuzuru miji kadhaa Amerika kati ya Agosti 26 na Oktoba 20 katika juhudi za kuwafikia Wakenya wanaoishi ughaibuni.