LALAMA za vijana kutekwa nyara katika eneo la Pwani zimezidi kuibuka, huku familia zilizoathirika zikiitaka serikali kueleza waliko wapendwa wao.
Suala hilo limefika katika Seneti, ambapo Jumanne, Seneta maalumu, Bi Shakila Abdalla aliwasilisha ombi kwa Kamati ya Usalama wa Taifa, Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni, akitaka uchunguzi kuhusu ongezeko la visa vya watu kutoweka katika Kaunti ya Lamu.
Kulingana na ombi lake, karibu watu 55 kutoka maeneo ya Kizingitini, Mbwajumwali, Tchundwa, Myabogi, Pate na Siyu waliripotiwa kutoweka kati ya Septemba na Oktoba 2026 chini ya mazingira yasiyoeleweka.
Maafisa wa usalama kaunti hiyo wanadai uchunguzi wa awali ulionyesha baadhi ya waliotoweka huenda walivuka mpaka na kuingia Somalia, ambako wanashukiwa kujiunga na kundi la wanamgambo wa Al-Shabaab.
Hata hivyo, familia zao zinadai wapendwa wao walitekwa na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa polisi.
“Visa hivi vimezidisha hofu, wasiwasi na hali ya kutokuwa na uhakika katika jamii na vinaonyesha umuhimu wa uchunguzi wa kina, uwajibikaji na taarifa za haraka kwa familia zilizoathirika,” alisema Bi Abdalla.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Pwani Ali Nuno alikanusha madai ya kuhusika kwa maafisa wa usalama, akisema ni visa viwili pekee, kimoja Lamu na kingine Mombasa, vilivyoripotiwa rasmi.
“Hatufahamu visa vingine wanavyovizungumzia. Ikiwa wana taarifa, wajitokeze na kuviripoti,” alisema Nuno, kwenye mahojiano na Taifa Leo.