Rais William Ruto ametangaza kuwa walimu 50,000 watapandishwa vyeo katika mwaka huu wa kifedha, huku serikali ikitenga Sh4 bilioni kutekeleza zoezi hilo.
Rais alitoa ahadi hiyo alipofunga mkutano wa wakuu wa shule za sekondari na msingi Kenya (KECSHA) mjini Mombasa, akisema hatua hiyo itakuwa mojawapo ya mipango mikubwa zaidi ya kupandisha vyeo walimu ndani ya mwaka mmoja.
Alisema Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) tayari imeidhinisha mwongozo mpya wa kupandisha vyeo walimu, uliokubaliwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) pamoja na vyama vya walimu.
“Katika mwaka huu wa kifedha, walimu 50,000 watapandishwa vyeo. Hii ni hatua muhimu katika kuimarisha taaluma ya ualimu,” alisema.
Rais aliongeza kuwa serikali itatoa Sh4 bilioni kusaidia utekelezaji wa mwongozo huo na kuwezesha walimu wengine kupanda ngazi za kazi.
Pia alitangaza kuwa serikali itaajiri walimu wengine 20,000 mwezi Desemba 2026, baada ya kuajiri 100,000 katika kipindi cha miaka minne iliyopita.
Katika hatua nyingine, Rais aliagiza Wizara ya Elimu kushirikiana na KECSHA kuandaa mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Elimu ya Msingi ili kuweka msingi wa kisheria wa shule za elimu jumuishi.
Alipatia wizara hiyo na chama hicho siku 90 kuwasilisha mapendekezo yatakayoshughulikia usimamizi, ajira na ufadhili wa shule hizo.
Alisema wakuu wa shule sasa wanasimamia wanafunzi kuanzia elimu ya chekechea hadi Gredi 9, na hivyo mfumo wa sasa unahitaji kuimarishwa ili kuendana na majukumu yao.