Rais William Ruto ameanza kuimarisha ushirikiano wa kisiasa kati ya UDA na ODM Nairobi, baada ya kukutana na viongozi wa mashinani na wanasiasa wapatao 1,500 kutoka vyama hivyo katika Ikulu ya Nairobi.
Mkutano huo uliwaleta pamoja viongozi waliochaguliwa na wagombeaji wanaotaka kuwania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Lengo kuu lilikuwa kuunganisha mifumo ya vyama hivyo, kuratibu kampeni na kuweka mikakati ya kuhakikisha vyama vinapata ushindi katika Kaunti ya Nairobi.
Ruto aliandamana na mwenyekiti wa kitaifa wa ODM Gladys Wanga, Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed na viongozi wengine wa vyama hivyo.
Rais aliwataka viongozi hao kuunganisha nguvu zao na kuimarisha uhamasishaji kuanzia mashinani hadi vituo vya kupigia kura ili kuhakikisha ushirikiano huo unazaa matunda katika uchaguzi ujao.
Mkutano huo ulifanyika huku vyama hivyo vikijaribu kugeuza ushirikiano wao katika serikali jumuishi kuwa nguvu ya kisiasa katika jiji mkuu, ambako kuna wapigakura 2,743,155.
Mabadiliko ya hivi majuzi ya kisiasa yamefanya hesabu za uchaguzi Nairobi kuwa tata zaidi. Gavana Johnson Sakaja alihama UDA na kujiunga na ODM, huku Mbunge wa Kasarani Ronald Karauri akijiunga na chama tawala.
UDA ilisema ina matumaini kuwa ushirikiano huo utawezesha kupata ushindi mkubwa Nairobi mwaka 2027.