Watu watatu wamethibitishwa kufariki dunia huku wengine 11 wakiokolewa wakiwa na majeraha mabaya baada ya ukuta kuporomoka katika eneo la ujenzi jijini Nairobi Jumamosi.
Serikali ya Kaunti ya Nairobi ilisema timu za uokoaji kutoka mashirika mbalimbali zilikuwa zikiendelea kuwatafuta wafanyakazi wengine wanane ambao hawakuwa wamepatikana kufikia wakati wa kutolewa kwa taarifa hiyo.
Tukio hilo lilitokea takriban saa tano na nusu asubuhi katika eneo la Riverside.
Kwa mujibu wa ripoti ya hali iliyotolewa na Afisa Mkuu wa Kaunti anayesimamia Usimamizi wa Maafa na Uratibu, Bramwell Simiyu, wafanyakazi 39 walikuwa katika eneo hilo wakati ukuta ulipoporomoka.
“Wafanyakazi 22 wamepatikana. Kati yao, 11 waliokolewa wakiwa hai kutoka kwenye vifusi na kupelekwa katika hospitali za karibu wakiwa na majeraha mabaya, huku wengine 11 wakithibitishwa kuwa salama na hali zao kuwa nzuri katika eneo la tukio,” alisema Bw Simiyu.
Aliongeza kuwa watu watatu walithibitishwa kufariki dunia na shughuli za kuopoa miili yao zilikuwa zikiendelea.
Timu za uokoaji zilikuwa zikiendelea kuondoa vifusi huku zikishirikiana na hospitali za karibu kubaini iwapo wafanyakazi hao wanane wasiojulikani walipo walikuwa wamepelekwa huko.
.Hakukuwa na orofa za juu zilizokuwa zimejengwa wakati ukuta huo ulipoporomoka.
Timu za usimamizi wa maafa za Kaunti ya Nairobi, zikishirikiana na mashirika ya kitaifa ya kukabiliana na dharura, zilizingira eneo la tukio ili kurahisisha shughuli za uokoaji na kulinda usalama wa wananchi.