Je, umewahi kufikiria kuzuia ndoa kwa kutoa taarifa za uongo ili wawili wasifunge harusi?
Sheria ya Ndoa ya Kenya inaonya dhidi ya tabia hiyo. Mtu anayetoa taarifa za uongo katika notisi ya kufunga ndoa au kupinga ndoa inayotarajiwa anaweza kufungwa hadi miaka miwili au kutozwa faini ya Sh2 milioni, au adhabu zote mbili.
Hii ina maana kuwa kutoridhishwa na mchumba wa mtu si sababu ya kubuni madai ili kuvuruga mipango ya harusi.
Kifungu cha 86 cha Sheria ya Ndoa kinaweka wazi kuwa mtu anayetoa taarifa ya uongo katika notisi ya nia ya kufunga ndoa au notisi ya kupinga ndoa anatenda kosa.
Hata hivyo, sheria inamlinda mtu ambaye alikuwa na sababu za msingi za kuamini kuwa taarifa aliyotoa ni ya kweli wakati alipoiwasilisha.
Kwa hivyo, mtu mwenye wasiwasi wa kweli kuhusu ndoa fulani anapaswa kutoa taarifa sahihi badala ya kutumia uongo kama silaha ya kulipiza kisasi.
Sheria pia inaweka adhabu kali kwa wanaohusika na ndoa za watoto. Mtu anayemuoa au kumwoa mtu aliye chini ya umri wa chini unaoruhusiwa anaweza kufungwa hadi miaka mitano au kutozwa faini ya Sh1 milioni, au vyote viwili.
Vilevile, kufunga ndoa kati ya watu walio katika uhusiano wa kindugu uliopigwa marufuku ni kosa linaloweza kumfanya mhusika afungwe hadi miaka mitano au kutozwa faini ya Sh300,000.