RAIS William Ruto Jumapili alimjibu Kiongozi wa Linda Mwananchi Edwin Sifuna, kuhusu madai kwamba mavazi aliyovalia kwenye harusi ya bintiye Charlene Chelangat Tanzania yaligharimu mamilioni ya pesa.
Kiongozi wa nchi alisema wakosoaji wake wanapaswa kuacha mambo madogo na kujadili sera na mipango ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika ibada ya kanisa mjini Narok Jumapili, Rais Ruto alitetea mtindo wake wa mavazi akisema ni uamuzi wake binafsi na kwamba yeye humakinikia kila jambo analofanya, ikiwemo jinsi anavyovaa.
“Kwa nini wanalalamikia mavazi yangu? Hilo linawahusu nini?” akauliza Rais Ruto.
Alisema baadhi ya wakosoaji wake wamezidisha makadirio ya gharama ya mavazi aliyovaa kwenye harusi ya bintiye iliyofanyika Mwanza, Tanzania, Novemba 6.
Rais aliongeza kuwa watu wanaotaka kuleta mabadiliko duniani huanza kwa kujipanga katika mambo madogo ya kila siku.
“Watu wanaobadilisha dunia huanza kwa mambo madogo kama kutandika vitanda vyao asubuhi,” akaongeza.
Alitumia fursa hiyo kuwashambulia wapinzani wake kwa kuangazia mavazi badala ya kujadili masuala muhimu yanayokabili nchi.
“Kuna tofauti gani kati ya wanaolalamikia fulana na wewe unayetoa maoni kuhusu koti, saa na viatu? Tuachane na mambo madogo na tukabiliane kuhusu manifesto, sera na mipango ya kuisukuma nchi mbele,” akasema.
Seneta Sifuna alikuwa amedai kuwa baadhi ya mavazi ya Rais kwenye harusi hiyo yalikuwa na thamani ya Sh80 milioni. Alidai koti alilovaa liligharimu Sh20 milioni, saa Sh30 milioni na viatu Sh20 milioni.