KAUNTI ya Lamu, iliyo maarufu kwa kuwatunza punda kwa taadhima, imepiga hatua zaidi katika juhudi hizo kwa kuzindua eneo rasmi la kuzika wanyama hao punde wanapofariki.
Sehemu hiyo ambayo imezungushiwa ua wa ukuta ilifunguliwa mwishoni mwa wiki katika eneo la Kandahar lililo viungani mwa mji wa kale wa Lamu kisiwani.
Litatumiwa pia kuzika wanyama wengine wanaofugwa nyumbani wanapokufa.
Hatua hiyo ilifanikishwa kupitia kwa mradi uliofadhiliwa na shirika la Donkey Sanctuary Kenya kwa ushirikiano na Serikali ya Kaunti ya Lamu kupitia Idara ya Mifugo na Manispaa ya eneo hilo.
Katika Kaunti ya Lamu, punda ni nguzo kuu ya uchumi, usafiri na utamaduni wa wenyeji kwa kuwa vichochoro vya mji wa kale wa Lamu ni vyembamba na magari hayatumiki kisiwani.
Kisiwa cha Lamu pekee kina zaidi ya punda 3,000.
Mkurugenzi wa Donkey Sanctuary Kenya, Dkt Solomon Onyango alisema kuzinduliwa kwa eneo maalumu la kuzika punda na mifugo wengine kisiwani Lamu ni hatua muhimu katika kudhibiti afya ya umma, uhifadhi wa mazingira na heshima kwa wanyama.
Afisa wa shirika hilo mjini Lamu, Bw Sam Kimeli, aliitaja hatua hiyo kuwa miongoni mwa mambo yanayodhihirisha wazi jinsi haki za wanyama zinavyozingatiwa.
Mkurugenzi wa Idara ya Mifugo katika Serikali ya Kaunti ya Lamu, Dkt Felix Rachuonyo alifafanua kuwa mizoga ya wanyama inapoachwa wazi au kutupwa ovyo huleta harufu mbaya na kuvutia nzi na vimelea vinavyoweza kusambaza…