VIONGOZI wa upinzani jana walifanya mikutano ya kisiasa katika Kaunti za Kisii na Nyamira, siku chache baada ya Rais William Ruto kukamilisha ziara ya siku nne katika eneo la Gusii, ambako alizindua miradi mbalimbali ya serikali.
Ziara hiyo ya upinzani ilionekana kuwa juhudi za kukabiliana na kampeni za kisiasa za Kenya Kwanza, huku viongozi hao wakiwataka wakazi wakatae kumchagua Rais Ruto tena mwaka ujao.
Walioshiriki katika mikutano hiyo ni kiongozi wa Jubilee Fred Matiang’i, Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro wa People's Party of Kenya (PPK), kiongozi wa People's Liberation Party (PLP) Martha Karua na Gavana wa Siaya James Orengo.
Viongozi hao walionya wakazi dhidi ya kushawishiwa na miradi ya maendeleo ambayo walisema Rais Ruto anaitumia kama chambo cha kutafuta muhula wa pili.
Wakihutubia wananchi katika mzunguko wa Capital, Kisii kabla ya kuelekea Keumbu na Keroka, viongozi hao walisema upinzani utabaki na umoja ili kuhakikisha Rais anaondolewa mamlakani.
“Walisema hatutakanyaga hapa. Hapa ni wapi? Kuna mtu anaweza kunizuia kurudi nyumbani? Rais aelewe kuwa sisi watu wa Gusii hatuuzwi na hakuna kiwango cha pesa kinachoweza kubadilisha msimamo wetu wa kumwondoa mamlakani,” akasema Dkt Matiang’i.
Alionya viongozi wa eneo hilo wanaomuunga Rais Ruto dhidi ya kuwasaliti wananchi kwa sababu ya pesa wanazopewa.
“Wasijaribu kuwauza watu wetu kwa kutumia pesa zilizoibwa na hongo wakicheza na maisha ya watu wetu.