MAMIA ya wafanyakazi wa Kiwanda cha nguo cha Samyong kilichoko Athi River, Kaunti ya Machakos Jumatatu walipata pigo baada ya moto mkubwa kuteketeza sehemu ya kiwanda hicho Jumapili usiku.
Moto huo ulizuka katika eneo la Gimu, Mavoko, kando ya Barabara Kuu ya Nairobi-Mombasa, na kusambaa katika sehemu mbalimbali za kiwanda hicho.
Mali iliyoharibiwa ni pamoja na majengo na vifaa vinavyotumika kiwandani, huku thamani kamili ya hasara iliyosababishwa na mkasa huo ikiwa bado haijabainika.
Tukio hilo limezua wasiwasi kuhusu hatima ya mamia ya wafanyakazi wanaotegemea kiwanda hicho kujikimu kimaisha, huku kukiwa na maswali kuhusu uwezekano wa shughuli za uzalishaji kurejelewa.
Shirika la Msalaba Mwekundu nchini lilisema moto huo ulidhibitiwa kufuatia juhudi za pamoja za wazimamoto na mashirika mengine ya kukabiliana na majanga ya dharura.
Katika taarifa yake Jumatatu asubuhi, shirika hilo lilithibitisha kuwa hakuna mtu aliyejeruhiwa.
"Moto umedhibitiwa na hakuna majeruhi walioripotiwa. Tathmini ya hali itafanywa baadaye leo," likasema taarifa ya shirika hilo.
Wazima moto kutoka Mavoko, Kaunti ya Machakos na Nairobi walishirikiana na maafisa wa Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS), polisi na Msalaba Mwekundu katika juhudi za kuzima moto huo.
Chanzo cha moto huo hakikuwa kimejulikana kufikia Jumatatu, huku uchunguzi ukitarajiwa kufanywa na mamlaka husika.
Mbali na hasara ya mali, tukio hilo linatarajiwa kuathiri wafanyakazi na biashara nyingine zinazotegemea shughuli za kiwanda hicho.