MAPAMBANO ya kuwania ubabe wa kisiasa miongoni mwa viongozi wa jamii ya Wamaasai yanazidi kupamba moto kadri uchaguzi mkuu wa 2027 unavyokaribia, uhasama wa hivi punde ukiwa kati ya Gavana wa Narok Patrick Ntutu na Mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo.
Uhasama kati ya viongozi hao wawili wa UDA ulijitokeza wazi Jumamosi wakati wafuasi wao walipopigana katika makala ya nne ya tamasha za utamaduni wa Wamaasai katika eneo la Sekenani, Kaunti ya Narok.
Vurugu hizo zilizoshuhudiwa na Rais William Ruto pamoja na viongozi wengine zilitatiza hafla iliyolenga kuadhimisha utamaduni wa jamii hiyo na kuibua wasiwasi kuhusu tofauti za kisiasa zinazoweza kuhatarisha umoja wa Wamaasai katika kaunti za Narok, Kajiado na Samburu.
Tofauti hizo zinaendelea wakati jamii hiyo ikikosa kiongozi mmoja mwenye ushawishi mkubwa kama ule wa aliyekuwa Mbunge wa Narok Kaskazini na Waziri William Ole Ntimama, aliyefariki Septemba 1, 2016.
Tangu kifo chake, viongozi mbalimbali wamekuwa wakishindania nafasi ya kuwa msemaji mkuu wa jamii hiyo, huku magavana, wabunge na maseneta wakijaribu kujijengea ushawishi wa kisiasa.
Katika Kaunti ya Narok, uhasama kati ya Bw Ntutu na Bw Tongoyo ulianza kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 wakati Dkt Ruto alipoingilia kati kuzuia mgawanyiko ndani ya UDA na kumuidhinisha Bw Ntutu kuwa mgombeaji wa kiti cha ugavana kupitia mkataba wa kisiasa.