ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua ametangaza kampeni kali za kuhakikisha chama chake cha DCP kinatwaa kiti cha ugavana wa Nairobi katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Bw Gachagua amesema DCP itatoa mgombeaji atakayefanikisha mageuzi na kurekebisha changamoto zinazokabili jiji kuu, huku akipuuza uwajibikaji wa Gavana wa sasa Johnson Sakaja na utendakazi wa Mbunge wa Kasarani Ronald Karauri.
Kufikia sasa, Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya ndiye mwanasiasa pekee ambaye ametangaza nia ya kuwania kiti hicho kupitia tiketi ya DCP.
Bw Gakuya, ambaye yuko katika muhula wake wa tatu bungeni, ni mshirika wa karibu wa Bw Gachagua, ingawa kiongozi huyo hajatangaza hadharani kama anamuunga kwa ugavana.
"Gavana atakayeirekebisha Nairobi atatoka DCP na nilimwambia Sakaja kwamba alikuwa akitumiwa kunipiga vita na kwamba hatimaye angetumiwa kisha kutupwa. Hata aliapa kiapo cha kisheria kuunga kuondolewa kwangu mamlakani lakini baadaye akajiondoa. Sasa ametupwa na Karauri kuletwa," akasema Bw Gachagua, akionekana kumrejelea Rais William Ruto kama aliyemtumia gavana huyo.
"Ndani ya ODM, (Rais William Ruto) anamuunga mkono Aladwa. Sasa Sakaja hana pa kuenda. Agosti mwaka ujao, wafuasi wangu watakuja kumwondoa madarakani. Kwa kuwa sasa umeachwa, basi umeisha," akaongeza.
Bw Gachagua alikuwa akizungumza wakati wa kufungua rasmi ofisi za DCP jijini Nairobi. Mnamo Disemba mwaka jana,
Bw Gachagua alitangaza mpango wa kugawana maeneo ya kisiasa kati ya DCP na chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka.