MAURICIO Pochettino anatua ugani Old Trafford akiwa na sifa ya kuwa kocha asiyependa masihara, anayekumbatia maandalizi kabambe kabla ya kila msimu na anayetaka wachezaji wote kuwa katika hali thabiti kiakili na kimwili kila wakati.
Manchester United wameajiri mkufunzi huyo raia wa Argentina hadi Juni 2029 kuchukua nafasi ya Michael Carrick aliyetimuliwa baada ya kikosi kusajili msururu wa matokeo duni muhula huu.
Kwa mujibu wa difenda wa zamani wa Tottenham Toby Alderweireld, Pochettino ni kocha shupavu aliye na msimamo imara katika masuala ya usimamizi na mwenye uwezo wa kupata kilicho bora kutoka kwa kikosi chake iwapo kila mmoja atajituma katika majukumu yake.
Alderweireld, 37, alinolewa na Pochettino kwa miaka minne huko Tottenham Hotspur na alishuhudia kikosi hicho kikifanikiwa kutinga fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kumaliza kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika nafasi ya pili.
“Ni mkufunzi anayefikika kwa urahisi lakini sharti ufuate masharti yake. Usipozingatia mipangilio yake na kukumbatia mbinu zake za ukufunzi, ni rahisi sana akuondoe mawazoni na utakosa nafasi ya kuchezea kikosi chake.”
“Anapenda sana wachezaji wanaohubiri lugha ya umoja na ushirikiano. Atamtema yeyote ambaye ni mbinafsi au anayejipenda na kujifikiria tu kwa kuweka mbele maslahi yake binafsi,” akasema Alderweireld.
“Ingawa anaheshimu kwamba mchezaji ana maisha yake nje ya uwanja wa soka, anapenda sana kufuatilia mambo madogo.