WAZIRI wa Elimu, Bw Julius Ogamba, amepinga madai ya msimamizi wa mtihani wa kitaifa wa shule za upili (KCSE) kutoka Kaunti ya Kwale, aliyeripoti kuwa alishambuliwa baada ya kukataa kushiriki katika njama ya kuruhusu udanganyifu katika m tihani huo unaoendelea.
Bw Ogamba alisema msimamizi huyo, Bw Julius Ndurya, aliyeshambuliwa na watu wasiojulikana mwendo wa saa nne usiku, alikuwa akirejea kutoka kwenye matembezi ya starehe, na kwamba tukio hilo halikuwa na uhusiano wowote na mitihani ya kitaifa inayoendelea.
“Mmoja wa maafisa wetu alienda eneo hilo kuchunguza suala hilo na nimeelezwa kuwa mwalimu huyo alikuwa akijivinjari saa nne usiku. Hapo ndipo aliposhambuliwa. Lakini tukio hilo halina uhusiano wowote na mitihani ya KCSE,” alisema Bw Ogamba.
“Tunachunguza ili kubaini kwa nini alidai kushambuliwa kwa sababu ya mitihani ilhali hakuwa hata karibu na kituo cha mitihani au shule,” alisema katika ofisi ya Naibu Kamishna wa Kaunti-ndogo ya Nyali, Jumatatu asubuhi.
Bw Ndurya, ambaye alikuwa msimamizi wa mitihani katika Shule ya Upili ya Vigurungani, eneo la Kinango, alipata majeraha ya kukatwa kichwani na kuvunjika mkono katika shambulizi la Jumatano jioni wiki iliyopita.
Akizungumza akiwa nyumbani kwake, alisema alishambuliwa baada ya kukataa kushiriki katika udanganyifu wa mitihani uliohusisha baadhi ya walimu na maafisa wa elimu wa eneo hilo.
Alidai kuwa alipewa Sh50,000 ili afiche ukiukaji wa taratibu za mitihani lakini akakataa.