SENETA wa Nairobi Edwin Sifuna na viongozi wa The Equitable Party (TEP) wamefikishwa mbele ya Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PPDT), wakilaumiwa kwa kutenga wanachama wa kawaida katika mchakato wa kubadili jina la chama hicho kuwa Linda Mwananchi Movement (LMM).
Mlalamishi Emmanuel Willyngtone Khamala, anasema wanachama walinyimwa nafasi ya kushiriki katika maamuzi muhimu kuhusu mwelekeo wa chama, ikiwemo kubadili jina na kuchagua viongozi wapya.
Amewasilisha kesi ya dharura kutaka utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa katika mkutano wa wajumbe wa kitaifa (NDC) wa Novemba 13 usitishwe hadi malalamishi yao yasikilizwe.
Kupitia wakili wake Danstan Omari, Bw Khamala anasema kamati kuu ya chama iliidhinisha jina jipya Oktoba 8 bila kushauriana ipasavyo na wanachama.
Anapinga pia kutangazwa kwa orodha ya viongozi wapya akisema wanachama hawakualikwa kuwachagua au kuwachunguza.
Bw Khamala, ambaye anasema ni mwanachama aliyesajiliwa kutoka Tongaren, Kaunti ya Bungoma, alijiunga na chama hicho Oktoba 11.
Anasema wanachama waliandika barua za malalamishi Oktoba 28 na Novemba 6 wakitaka maelezo kuhusu mabadiliko hayo, lakini hawakujibiwa.
Katika kesi hiyo, wakili Omari anasema maamuzi ya mkutano huo yanaweza kutekelezwa kabla ya wanachama kupata nafasi ya kueleza wasiwasi wao.
Katiba ya TEP inatambua mkutano wa wajumbe wa kitaifa kuwa chombo cha juu zaidi cha chama. Pia inahitaji marekebisho ya katiba kuungwa mkono na angalau theluthi mbili ya wajumbe wanaostahili kupiga kura.



