MZOZO kati ya Serikali ya Kaunti ya Mombasa na kampuni ya GulfCap Real Estate kuhusu mradi wa nyumba za bei nafuu wa Buxton Point umefichua maelezo ya ndani kuhusu makubaliano ya kimkataba kati ya pande hizo mbili.
Imebainika kuwa, pande hizo mbili zilikubaliana kaunti iwe na haki ya kupata asilimia 10 ya nyumba za makazi na maeneo ya biashara katika mradi huo, ambayo ni sawa na karibu nyumba 180 kati ya jumla ya 1,800 zilizopangwa kujengwa.
Wiki iliyopita, Kaunti ilitangaza kusimamisha shughuli za ujenzi ikilalamikia ukiukaji wa mkataba, hatua iliyofanya mkandarasi kwenda mahakamani kupinga hatua hiyo.
Hata hivyo, Novemba 12, Mahakama ya Mazingira na Ardhi Jijini Mombasa, ilikataa kutangaza kuwa ombi lililowasilishwa na kampuni ya Buxton Point Apartments Limited lilikuwa la dharura, na ikaahirisha uamuzi kuhusu ombi la kusimamisha utekelezaji wa notisi hiyo hadi baada ya kusikiliza pande zote.
Buxton Point Apartments Limited ni kampuni tofauti iliyoanzishwa na GulfCap kwa madhumuni maalumu ya kutekeleza mradi wa ukarabati na ujenzi upya wa makazi ya Buxton.
Nyaraka zilizowasilishwa mahakamani zinaonyesha kuwa, kampuni hiyo ndiyo inatekeleza ujenzi kwa ardhi yenye nambari ya usajili Mombasa Block XVII/1821, iliyokuwa ikijulikana awali kama Mombasa Block XVII/1776, chini ya makubaliano kati yake na Kaunti yaliyotiwa sahihi Januari 15, 2020.
Chini ya makubaliano hayo, mkandarasi alipewa jukumu la kutekeleza na kukamilisha mradi huo, huku kaunti ikitakiwa kutoa hatimiliki…