WATU tisa waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa baada ya majangili kuvamia wafugaji katika kijiji cha Janju, eneo la Banane, kaunti ndogo ya Lagdera, mpakani mwa Garissa na Isiolo Jumanne usiku.
Washambuliaji hao, wanaoshukiwa kuwa wezi wa mifugo kutoka Isiolo, waliiba mbuzi 1,500 na ngamia 60 baada ya kuwavamia wafugaji wakiwa wamelala.
Kamishna wa kaunti ndogo ya Lagdera Paul Langat, alisema hali ya wasiwasi imetanda eneo hilo huku maafisa wa usalama wakiwasaka washambuliaji na kutafuta mifugo walioibwa.
Miongoni mwa waliouawa ni mama mmoja, mtoto wake mchanga wa siku 14 na mtoto mwingine wa miaka 10.
Mkazi wa Modogashe, Adan Shukri, alisema eneo hilo halijakuwa na mashambulizi ya aina hiyo kwa muda mrefu.
Kiongozi wa wengi katika Bunge la Kaunti ya Garissa, Mohamed Abdi Farah, alitaka uchunguzi wa haraka, kurejeshwa kwa mifugo na hatua za kurejesha amani.
Aliwataka magavana wa Garissa na Isiolo kushirikiana na viongozi wa jamii kuanzisha mazungumzo ya kumaliza migogoro ya mara kwa mara na kuzuia vifo na kuhama kwa wakazi.