RAIS William Ruto jana alichora taswira ya nchi iliyo sawa, akisema kwa miaka minne iliyopita ameweka mpango wa kubadilisha Kenya kuwa taifa lenye uchumi imara huku akitaja uwekezaji wa Sh5 trilioni katika kipindi cha miaka 10 ijayo, ujenzi wa barabara na upanuzi wa huduma muhimu kama nguzo za safari hiyo.
Akihutubia kikao cha pamoja cha Bunge katika hotuba yake ya Hali ya Taifa 2026 jana, Rais alisema serikali imeweka msingi wa mabadiliko kupitia kilimo, afya, nyumba za gharama nafuu, elimu, ajira na miundombinu.
Huku akishangiliwa na wabunge na maseneta hasa wanaounga serikali, Rais Ruto alisema lengo lake ni kuhakikisha kila Mkenya ananufaika na maendeleo bila kujali eneo alikozaliwa, hali yake ya kifedha au jamii anayotoka.
“Ndoto yangu kuu ya kujenga Kenya ambako kila raia anahesabiwa, kila jamii inahisi kuwa sehemu ya taifa na hakuna Mkenya anayeachwa nyuma, inazidi kuwa halisi,” alisema.
Hotuba ya mwaka huu ilifanyika kwa utulivu tofauti na miaka miwili iliyotangulia wakati nchi ilikumbwa na maandamano dhidi ya serikali na ilihudhuriwa na idadi kubwa ya wabunge hasa wanaounga Serikali Jumuishi.
Kwa zaidi ya saa mbili, akipigia debe kauli mbiu mpya ya chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) ya Usawa ni Sawa, Rais alisema serikali inalenga kuondoa tofauti za maendeleo zilizokuwepo kwa muda mrefu, ambapo maeneo yaliyokuwa na barabara, viwanda na miundombinu mingine yalivutia uwekezaji zaidi huku jamii…