MWANAMUME mwenye umri wa miaka 26 aliyetoweka mjini Mombasa mwezi uliopita aliwahi kushtakiwa kwa kosa la kusajili watu kujiunga na kundi la kigaidi, lakini baadaye akaachiliwa huru na mahakama, imebainika.
Stakabadhi zilizowasilishwa katika Mahakama Kuu ya Mombasa zinaonyesha kuwa Ismail Yusuf Mohamed alikabiliwa na mashtaka yanayohusiana na ugaidi Januari 2022, miaka minne kabla ya kutoweka kwake.
Mohamed alishtakiwa katika kesi ya uhalifu iliyokuwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Malindi.
Hata hivyo, katika uamuzi uliotolewa Agosti 11, 2023, mahakama ilimuachilia huru baada ya kubaini kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha tuhuma zilizokuwa dhidi yake.
Kesi hiyo ya awali imeibuka katika ombi lililowasilishwa na shirika la kutetea haki za binadamu la Vocal Africa, ambalo linaitaka polisi kueleza aliko Mohamed aliyetoweka kwake Oktoba 31 mwaka huu.
Katika hati ya kiapo iliyowasilishwa mahakamani, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo, Bw Hussein Khalid, alisema Mohamed aliondoka nyumbani kwao eneo la Bondeni, Mombasa, kwenda kununua chakula cha jioni lakini hakurejea.
Kwa mujibu wa hati hiyo, Mohamed alitekwa nyara mwendo wa saa tano usiku nje ya mgahawa wa Bondeni Carmel’s Joint, kando ya Barabara ya Abdel Nasser, na watu waliokuwa wakimfuatilia kwa gari aina ya pickup.
Ombi hilo linadai kuwa, video za kamera za CCTV zinaonyesha wanaume hao wakishuka kwenye gari hilo, kumkamata Mohamed na kumwingiza kwa nguvu katika gari jeupe aina ya Toyota Land Cruiser kabla ya kuondoka…