TANGAZO la Rais William Ruto kuhusu malipo ya Sh15.07 bilioni kwa wakulima 680,000 wa kahawa na bonasi ya Sh1.2 bilioni kwa wakulima wa miwa ni hatua inayostahili kupongezwa.
Kiongozi wa nchi jana alitangaza malipo hayo alipotoa hotuba yake ya kila mwaka kwa Bunge ambapo pia alizungumzia mafanikio mengine ya serikali yake.
Rais alisema bei ya kahawa imeongezeka kutoka Sh69 hadi Sh130 kwa kilo, huku mapato ya kitaifa kutokana na mauzo ya kahawa nje ya nchi yakiongezeka maradufu kutoka Sh26 bilioni hadi Sh52 bilioni.
Aidha, wakulima wa miwa wanatarajiwa kupokea bonasi ya Sh1.2 bilioni kuanzia wiki ijayo.
Hizi ni habari njema kwa wakulima ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakikabiliwa na gharama kubwa za uzalishaji, bei duni za mazao, madeni na mifumo ya ushirika isiyowajibika.
Wakulima wa kahawa, hasa, wamevumilia misimu ya mavuno duni, ucheleweshaji wa malipo na changamoto za magonjwa pamoja na hali mbaya ya hali ya hewa.
Kuongezeka kwa bei ya kahawa na mapato ya mauzo ya nje kunaashiria kuwa mageuzi katika sekta hiyo yameanza kuzaa matunda.
Takwimu zinaonyesha uzalishaji wa kahawa uliongezeka kutoka tani 49,500 mnamo 2024 hadi tani 51,400 mnamo 2025.
Hata hivyo, ongezeko hili bado halitoshi kuifanya sekta hiyo kuwa na nguvu ikilinganishwa na uwezo wake wa kihistoria.
Serikali inapaswa kuhakikisha fedha zilizotangazwa zinawafikia wakulima wanaostahili bila kucheleweshwa, mapendeleo au mianya ya ufisadi.