MVUTANO kati ya Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino umechukua mkondo mpya baada ya wawili hao kuanza kurushiana lawama kuhusu nani alisaliti makubaliano yao ndani Linda Mwananchi.
Tofauti zao sasa zinaibua maswali kuhusu uongozi, uwaniaji wa urais na ugavana wa Nairobi, huku uchaguzi mkuu wa 2027 ukikaribia.
Bw Sifuna alivunja kimya chake mnamo Alhamisi alipomjibu Bw Owino, ambaye amemshutumu kwa kuvunja makubaliano yaliyopangwa awali kuhusu nafasi zao ndani ya Linda Mwananchi ambacho sasa ni chama cha kisiasa.
Mbunge huyo, ambaye ametangaza nia ya kuwania ugavana wa Nairobi, anadai kwamba wawili hao walikuwa wamekubaliana Bw Sifuna awe mgombeaji urais huku yeye akiongoza chama.
Hata hivyo, anasema mpango huo ulibadilishwa bila kushirikishwa wala kupewa maelezo. Akizungumza katika kipindi cha Jambo Kenya cha Radio Citizen, Bw Sifuna alisema alishangazwa na pendekezo la Bw Owino kwamba awe kiongozi wa chama huku yeye akichukua nafasi ya mgombeaji urais.
Alisema haelewi jinsi mbunge huyo anavyoweza kumwamini kuongoza nchi lakini akawa na dukuduku kuhusu uwezo wake wa kuongoza chama.
Kwa mujibu wa Bw Sifuna, makubaliano ya awali yaliwataka waache vyama vyao binafsi na kujiunga na chama kimoja ambacho kingewapa jukwaa la kutimiza malengo yao ya kisiasa.
Alisema baada ya kuchunguza vyama vilivyokuwepo, walichagua The Equitable Party (TEP), ambayo baadaye ilibadilishwa jina na kuwa Linda Mwananchi Movement.