KWA mara ya kwanza, idara ya Mahakama imechapisha takwimu zinazoonyesha idadi ya kesi zilizoamuliwa na kila jaji na hakimu katika mwaka uliotamatika Juni 2026.
Ripoti ya kurasa 328 kuhusu hali ya Mahakama na utoaji haki imetaja majina ya maafisa hao pamoja na idadi ya hukumu, maamuzi na maagizo mengine waliyotoa.
Hata hivyo, Idara ya Mahakama imesisitiza kuwa takwimu hizo si orodha hiyo haitokani na mashindano ya majaji kazini.
Katika Mahakama Kuu, Jaji Reuben Nyakundi aliongoza kwa kuamua kesi 1,791.
Alifuatiwa na Alfred Mabeya aliyeshughulikia kesi 968, Teresa Odera (956), Richard Mwongo (913), Teresia Matheka (906) na Kizito Magare (904).
Majaji wengine waliokuwa na idadi kubwa ya maamuzi ni Diana Kavedza (824), Mwanaisha Saida (778), Lucy Gitari (745), huku Helene Namisi na Florence Muchemi wakiwa na kesi 744 kila mmoja.
Katika Mahakama ya Rufaa, jumla ya kesi 2,394 ziliamuliwa na majopo ya majaji.
Jopo la Kisumu lililoongozwa na majaji Hellen Omondi, Luka Kimaru na Milton Makhandia liliongoza kwa kesi 172.
Katika Mahakama ya Ajira na Mahusiano Kazini, Jaji Jemima Keli aliongoza kwa maamuzi 499, akifuatwa na Monica Mbaru na Stella Rutto waliokuwa na 484 kila mmoja.
Katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi, Emmanuel Washe aliongoza kwa kesi 456, akifuatwa na Fred Nyagaka (455) na David Mugo (442).