RAIS William Ruto amewaonya vijana dhidi ya kuruhusu wanasiasa kuwatumia kama wanablogu au wahuni wa kuvuruga mikutano, akitangaza mpango wa nguzo tano unaolenga kuwapa ajira na kuwawezesha kiuchumi.
Akizungumza siku ya pili ya ziara yake katika eneo la Magharibi mwa Kenya Ijumaa, Rais alisema vijana wanapaswa kujikita katika kutafuta fursa za kujipatia riziki badala ya kutumiwa katika mapambano ya kisiasa.
Alisema mpango wake unalenga kuwawezesha vijana kupitia elimu, mafunzo ya kazi, mitaji, zabuni za serikali na ajira katika sekta mbalimbali.
Nguzo ya kwanza ni mfumo mpya wa ufadhili wa vyuo vikuu, ambao alisema utahakikisha wanafunzi wanaendelea na masomo bila kukatizwa na ukosefu wa karo.
Pili, serikali inalenga kuwaingiza zaidi ya vijana 100,000 katika mafunzo ya kazi, ambapo kila mmoja atalipwa Sh25,000 kabla ya kupata ajira za kudumu.
Kupitia mpango wa Nyota, serikali tayari imetoa Sh50,000 kwa kila mmoja wa vijana zaidi ya 130,000 wenye ujuzi lakini wasio na ajira ili kuanzisha biashara.
Ruto alisema serikali inatafuta vijana wengine 200,000 watakaonufaika na mpango huo.
Nguzo ya nne ni kuwaunganisha vijana na zabuni za serikali kupitia mpango wa Nyota-AGPO. Vijana watasajiliwa, kupewa mafunzo ya wiki 10 na kusaidiwa kusajili kampuni zao bila malipo.
Rais alisema serikali italipa bidhaa zitakazowasilishwa ndani ya siku 60.
Nguzo ya tano ni ajira kupitia ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, masoko, mabweni, vituo vya teknolojia na ajira…