Chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kati (Kuppet) kimepinga mpango wa Rais William Ruto wa kuanzisha mfumo wa shule jumuishi, kikisema hautatatua changamoto za elimu nchini.
Katibu Mkuu wa Kuppet Akelo Misori alisema mpango huo hauna msingi wa kisheria na unaweza kuvuruga usimamizi wa shule, hasa katika Gredi 7, 8 na 9.
Kuppet imekuwa ikishinikiza shule za Sekondari Msingi (JS)ziwe na usimamizi wake tofauti na shule za msingi, ikisema walimu wake hawawezi kuongozwa na wakuu wa shule za msingi.
“Kuendesha mfumo huu bila marekebisho ya Katiba ni kufanya majaribio,” alisema Misori.
Alisema Sekondari Msingi hufuata mtaala wa kiwango cha shule za upili, hivyo si vyema kuziweka chini ya wakuu wa shule za msingi ambao wamefunzwa kusimamia elimu ya msingi.
Misori alisema kuwa hata kama shule hizo ziko katika eneo moja, zinaweza kuwa na usimamizi tofauti, akitaja shule ya msingi ya Chuo Kikuu cha Kenyatta ambayo huendeshwa kivyake licha ya kuwa ndani ya chuo hicho.
Pia alionya kuwa baadhi ya walimu waliofunzwa kufundisha masomo ya msingi wamepewa masomo ya sayansi na kiufundi katika JS bila kuwa na sifa zinazohitajika.
Rais Ruto aliagiza Wizara ya Elimu kushirikiana na Chama cha Wakuu wa Shule Jumuishi nchini (Kecsha) kuandaa mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya Elimu ya Msingi ndani ya siku 90.