SERIKALI ya Rais William Ruto imeibua wasiwasi kuhusu usalama wa nchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027, ikionya kuwa kuongezeka kwa magenge ya wahalifu, joto la kisiasa, siasa za kikabila na matamshi ya uchochezi kunaweza kufanya Kenya kuwa katika hatari ya machafuko.
Katika ripoti ya hali ya usalama nchini iliyowasilishwa Bungeni na Rais Ruto wakati wa hotuba yake ya Mustakabali wa Taifa, serikali inasema ushindani wa kisiasa unaozidi kupamba moto unaweza kudhoofisha umoja wa kitaifa na kuhatarisha amani kabla ya uchaguzi.
Ripoti hiyo inayohusu kipindi cha Septemba 2025 hadi Agosti 31, 2026, inaeleza kuwa mwelekeo wa kisiasa kuelekea uchaguzi wa 2027 ndio wasiwasi mkubwa zaidi kwa idara za usalama.
Serikali inasema mchujo wa vyama, mapitio ya mipaka ya maeneo ya uchaguzi na usajili wa wapigakura ni baadhi ya hatua zinazoweza kuchochea ushindani mkali na hata vurugu.
"Safari ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027 ndiyo wasiwasi mkuu. Kura za mchujo za vyama, mapitio ya mipaka na usajili wa wapigakura vitaongeza ushindani wa kisiasa, huku hali katika kipindi hiki ikionyesha hatari kubwa ya vurugu zinazochochewa katika hatua hizo," inasema ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa serikali, kipindi hiki hushuhudia mgawanyiko mkubwa wa kisiasa, kutovumiliana kati ya mirengo hasimu na juhudi za wanasiasa kuchochea wafuasi dhidi ya wapinzani wao.
Ripoti hiyo pia inadai kuwa baadhi ya wanasiasa wametumia vurugu katika maeneo mbalimbali kujionyesha kuwa na…