KUONDOKA kwa vinara wakuu wa upinzani katika mkutano na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumempa Rais William Ruto nafasi nyingine ya kuwashambulia kisiasa, akitumia mgogoro huo kuonyesha kuwa wapinzani hawana umoja, mgombeaji wala ajenda ya pamoja kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Vinara hao, wakiongozwa na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, waliondoka kwenye mkutano wa Novemba 19 baada ya kupinga utaratibu wa majadiliano na mada ambazo IEBC ilikuwa imepanga kuwasilisha.
Walioandamana nao ni aliyekuwa Jaji Mkuu David Maraga, kiongozi wa People's Liberation Party Martha Karua, Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu Justin Muturi na kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa, miongoni mwa wengine.
Hata hivyo, hatua hiyo imegeuza mjadala kutoka kwa madai yao kuhusu maandalizi ya uchaguzi na kuuelekeza kwenye uwezo wa upinzani kuendesha mazungumzo na kuunda mkakati mmoja wa kumng'oa Ruto mamlakani.
Rais hakupoteza muda kutumia fursa hiyo. Akiwa katika ziara yake ya Magharibi mwa Kenya, aliwashambulia wapinzani akiwataka waache kuilaumu IEBC na badala yake wajipange kushindana naye katika uchaguzi.
'IEBC haina kura, kura ziko kwa wananchi,' alisema Ruto, akiwakosoa viongozi hao kwa kuonekana kuhusisha tume na mizozo yao ya kisiasa.
Pia, aliwataka wapinzani waache kuzunguka wakilalamika kuhusu tume hiyo na badala yake waamue watakayemsimamisha kugombea urais, sera watakazotumia na…