WATU wengi wanapoachana au kutengana katika ndoa, hudhani kuwa kila mmoja anapaswa kuanza maisha yake bila kuwajibika tena kwa mwenzake.
Hata hivyo, sheria inatambua kuwa kuna mazingira ambapo mtu anaweza kuamriwa kuendelea kumtunza mchumba wake, hata baada ya ndoa kuvunjika.
Sheria inapatia mahakama mamlaka ya kutoa agizo la matunzo kwa mke, mume au mpenzi wa zamani iwapo kuna sababu zinazohalalisha hatua hiyo.
Lengo ni kuhakikisha kuwa mtu ambaye anastahili kupata msaada wa kifedha haachwi bila mahitaji muhimu kutokana na mchumba wake kukwepa wajibu.
Moja ya sababu zinazoweza kumfanya mtu aagizwe kulipa matunzo ni kukataa au kupuuza wajibu wa kumtunza mchumba wake kama sheria inavyotaka.
Hii ina maana kuwa mtu hawezi kujiondoa katika wajibu wake kwa makusudi na kumwacha mwenzake akihangaika kutafuta mahitaji ya msingi.
Pia, mahakama inaweza kutoa agizo hilo pale ambapo mmoja wa wanandoa amemtelekeza mwenzake. Agizo hilo linaweza kuendelea kutumika kwa muda wote ambao hali ya kutelekezwa inaendelea.
Hivyo, mtu anayeondoka nyumbani na kuacha mwenzi wake bila msaada anaweza kukabiliwa na hatua za kisheria.
Matunzo yanaweza pia kuamriwa wakati kesi za ndoa zinaendelea mahakamani.
Hii ni muhimu kwa sababu kesi za kutengana au talaka zinaweza kuchukua muda, huku mmoja wa wanandoa akiwa hana uwezo wa kujikimu bila msaada wa mwenzake.
Aidha, mahakama inaweza kuamua kuhusu matunzo wakati wa kutoa uamuzi wa kutengana au kuvunja ndoa, au hata baada…