WATU wawili wamefariki huku wengine wawili wakijeruhiwa vibaya kufuatia mlipuko unaoshukiwa kusababishwa na gesi ya kupikia katika mkahawa karibu na Lango la 8 la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari nchini (KPA), Mombasa.
Kamanda wa Polisi wa Kaunti ya Mombasa, Bi Stella Cherono, alithibitisha mkasa huo wa asubuhi na kusema kuwa uchunguzi umeanzishwa kubaini chanzo halisi cha mlipuko huo.
“Majira ya saa nne na dakika 50 asubuhi, tukio lilitokea katika eneo la Bandari ya Kilindini, Docks. Kibanda cha chakula kilishika moto, na tunashuku huenda chanzo kilikuwa kuvuja kwa gesi kutoka kwenye mtungi, hali iliyosababisha moto huo. Kwa bahati mbaya, watu wawili walifariki katika tukio hilo huku wengine wawili wakikimbizwa hospitalini,” alisema Bi Cherono.
Kwa mujibu wa kamanda huyo wa polisi, magari ya kuzima moto kutoka KPA na Serikali ya Kaunti ya Mombasa yalifika eneo la tukio kwa haraka na kufanikiwa kudhibiti moto huo, hivyo kuhakikisha maeneo mengine ya bandari hayakuathirika.
“Uchunguzi unaendelea ili kubaini kwa kina kilichotokea. Waliofariki ni wanawake wawili waliokuwa wakifanya kazi katika vibanda hivyo vya chakula, huku waliojeruhiwa wakiwa mmiliki wa kibanda na mfanyakazi mwingine,” aliongeza Bi Cherono.
Aliwahakikishia wananchi kuwa wachunguzi watafanya kila juhudi kubaini chanzo cha mkasa huo, akisema kuwa uchunguzi utahusisha pia kumtafuta mfanyabiashara aliyemuuzia mhusika mtungi wa gesi.
Mfanyabiashara, Bw Davis Mwalimu Mwangeka, ambaye mkewe Edith Mwangeka anaendesha mkahawa huo, alisimulia alivyopokea taarifa kuhusu…