VISA vya mauaji, ujambazi, uhalifu wa kiuchumi na wizi wa magari na mifugo, vimeongezeka nchini katika kipindi cha mwaka mmoja hadi Agosti 2026, ripoti mpya ya serikali imeonyesha.
Ripoti ya kila Mwaka kuhusu Hali ya Usalama Kitaifa, iliyowasilishwa bungeni na Rais William Ruto, inaonyesha kuwa visa 97,946 vya uhalifu viliripotiwa kwa polisi kati ya Septemba 2025 na Agosti 2026, ikilinganishwa na 97,366 katika kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.
Hii ni ongezeko la visa 580, sawa na asilimia 0.6.
Visa vya ujambazi viliongezeka kutoka 3,428 hadi 3,549, huku mauaji yakipanda kutoka 2,806 hadi 2,814.
Uhalifu wa kiuchumi uliongezeka kutoka 4,359 hadi 4,655, wizi wa magari kutoka 1,291 hadi 1,321 na wizi wa mifugo kutoka 2,336 hadi 2,430.
Hata hivyo, baadhi ya makundi yalishuhudia kupungua kwa visa.
Wizi wa kawaida ulipungua kutoka 16,763 hadi 16,161, uvamizi wa nyumba kutoka 5,350 hadi 4,654, huku uhalifu dhidi ya watu wengine ukishuka kutoka 24,531 hadi 23,564.
Licha ya takwimu hizo, maeneo mbalimbali nchini yamekumbwa na ongezeko la mashambulizi ya majambazi, mauaji na uvamizi wa nyumba, hali inayozua hofu miongoni mwa wananchi.
Jijini Kisumu, wakazi wamekuwa wakilengwa na majambazi wanaopora simu na vitu vya thamani, huku baadhi ya wahalifu wakitumia pikipiki kutekeleza uhalifu.
Mwanaharakati wa haki za raia na mwenyekiti wa Muungano wa Wakazi wa Kisumu, Audi Ogada, alisema wahalifu wamevamia mitaa na makazi ya watu.