NAIROBI ni jiji pekee Kenya litakaloandaa mechi za Kombe la Afrika (AFCON) 2027, hali iliyozua dhihaka kutoka kwa mashabiki wa soka barani Afrika mitandaoni jana.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilitangaza Jumamosi kuwa Kenya itatumia Nairobi pekee, huku Tanzania na Uganda wakipata miji mitatu na miwili mtawalia.
Tanzania itatumia Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar, huku Uganda ikitumia Kampala na Hoima. Makala hayo ya 36 yatafanyika Juni 19 hadi Julai 17, 2027.
Tangazo hilo lilizua mjadala kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya mashabiki wakihoji kwa nini Kenya, inayojivunia hatua kubwa kimaendeleo Afrika Mashariki, imeshindwa kupata miji mingine ya kuandaa mechi.
“Kenya ni simba wa karatasi,” aliandika mtumiaji wa X @KennedyMmar.
@MoiponeSenoe naye aliuliza: “Kenya itakuwa na mechi katika jiji moja? Hakuna viwanja Mombasa?”
Naye @CodeMetalai alisema: “Kenya ni simba mtandaoni lakini paka nyumbani.”
Hata hivyo, barua za zabuni ya pamoja ya Kenya, Uganda na Tanzania zinaonyesha kuwa Kenya awali ilikuwa imependekeza Nairobi na Eldoret kuwa miji ya kuandaa Afcon.
Nairobi ilikuwa imewasilisha Kasarani yenye uwezo wa kusitiri mashabiki 48,000 na Nyayo yenye viti 18,000 kama nyuga za kutumika.
Eldoret iliwasilisha uwanja wa Kipchoge Keino unaoweza kusitiri mashabiki 15,000, huku serikali ikipanga kuongeza idadi hadi 30,000.
Lakini CAF haikuitaja Eldoret katika orodha ya miji iliyotangazwa Jumamosi.