SERIKALI ya Kaunti ya Mombasa imeponea mzigo wa kuwarejeshea wakazi na wafanyabiashara kodi na ushuru iliyokusanya kwa kipindi cha mwaka mzima chini ya Sheria ya Fedha ambayo Mahakama Kuu imebaini kuwa ilitungwa kinyume na Katiba.
Katika hukumu iliyotolewa Novemba 20, Mahakama Kuu mjini Mombasa ilikiri kuwa serikali ya kaunti na Bunge la Kaunti zilikiuka wajibu wao wa kikatiba wa kuwashirikisha wananchi katika utungaji wa sheria.
Hata hivyo, mahakama ilisema kubatilisha ukusanyaji wa mapato ya mwaka mzima kungevuruga utoaji wa huduma za umma.
Mahakama ilikataa kubatilisha Sheria ya Fedha ya mwaka 2024 (Na. 6 ya 2024) wala kuamuru kurejeshwa kwa fedha zilizokusanywa, ikisema walalamishi walishindwa kuwataja wasafirishaji au wafanyabiashara waliolipa ushuru uliopingwa na kuwasilisha ushahidi wa malipo hayo.
“Kasoro niliyoibaini inahusu utaratibu uliofuatwa. Sijabaini kuwa ada yoyote mahususi ilitozwa nje ya mamlaka ya kaunti,” mahakama ilisema.
Sheria hiyo ilianza kutekelezwa Januari 1, 2025 na kutumika mwaka mzima.
Mahakama ilibainisha kuwa kaunti ilikuwa tayari imetumia mapato hayo kutoa huduma za umma, huku wafanyabiashara wakipata vibali, leseni na huduma nyingine badala ya malipo yao.
Mahakama pia iliwakosoa walalamishi kwa kusubiri hadi Aprili 2025 kuwasilisha kesi kupinga sheria ambayo tayari ilikuwa imeanza kutekelezwa, ikisema kuwa kufikia wakati huo wafanyabiashara wengi walikuwa tayari wamelipa.
Mashirika mbalimbali ya wafanyabiashara yaliwasilisha kesi hiyo Aprili 2025.