INAONEKANA chama cha Orange Democratic Movement (ODM) hakijui siri ya utongozaji. Ni siri ya wanaume wengi hasa, na hakuna uamuzi wowote wa mahakama unaomkataza mtu kuifichua. Nitakutobolea.
Nakusihi ujongee nikudokezee kwa matao ya chini. Sharti langu ni kwamba usiwaambie watu wa ‘pawa’ kule ODM.
Hatuwezi kuwafunza kila kitu. Acha kiwarambe kidogo.
Tangu hapo wajinga ndio waliwao. Na hawa wataliwa na Ulliam kwa raha zake, awatengezee mishikaki au kaimati.
Sijali, nitaketi kitako na kujionea sinema yenyewe.
Siri ya utongozaji ni kwamba, kabla hujapewa ‘mechi’ hufai kumuuliza mwenzako iwapo ana mtu au la. Unamtaka yeye, au mtu wake? Tumia akili nanii… Pia, usimwonyeshe kwamba umesalitika kwake kishenzi, yaani huna chaguo, akitaka akumalize.
Kisa na maana, huenda ukapewa jawabu usilopenda, likukatishe tamaa, janja zote ulizotembeza ziwe mbio za sakafuni ambazo kawaida huishia ukingoni. Kumbuka kukataliwa kubaya. Kuna safari ambazo hazifai kuvunjikia njiani kabla ya wino na karatasi kukutana.
Mtu akishaingia ‘boksi’, kisha umuulize iwapo ana ‘mtu’, hata akitoa jawabu lisilokupendeza, hatakuwa na sababu ya kutomuacha ‘mtu’ wake au kutoendelea na uhusiano huo na kukufuata kwa kuwa tayari amevuka ‘mshororo mwekundu’.
Hata akitaka kuondoka, unamkumbusha mmetembea pamoja safari ndefu sana, kwake kutaka kurejea alikotoka, au kuketi hapo tu kizembe, ni kufanya maamuzi ya kijinga, kitoto, au yote mawili. Aghalabu atakufuata shingo upande.