CHAMA cha Jubilee kimepata mabadiliko mapya baada ya naibu kiongozi wake Jeremiah Kioni kujiuzulu, akihitimisha uhusiano wake wa kisiasa wa miaka 11 na chama hicho kinachojiandaa kufanya mkutano maalumu wa wajumbe wiki ijayo.
Bw Kioni, aliyewahi kuwa Mbunge wa Ndaragwa na katibu mkuu wa zamani wa Jubilee, alitangaza kuondoka Alhamisi, siku moja baada ya chama kutoa notisi ya kuitisha Mkutano Maalumu wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) Desemba 3 katika Jockey Club, barabara ya Ngong, Nairobi.
Mkutano huo unatarajiwa kujadili ripoti za vitengo mbalimbali vya chama, kuchagua na kuidhinisha viongozi wa kitaifa, pamoja na mapendekezo ya mabadiliko ya katiba ya Jubilee.
Hatua hiyo inajiri huku chama hicho kikiendelea na mabadiliko ya uongozi chini ya aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i, ambaye anajiandaa kuwania urais katika uchaguzi wa 2027.
Katika barua yake ya kujiuzulu, Bw Kioni alisema uamuzi wake umetokana na kutafakari safari yake ya miaka 11 ndani ya Jubilee, akieleza kuwa chama hicho kilikuwa kama nyumbani kwake na kilimpa nafasi ya kuwatumikia Wakenya.
“Imekuwa miaka 11, safari ndefu na muhimu katika maisha yangu, ambayo naweza kuwa tayari kuipitia tena,” alisema.
Alimshukuru Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa uongozi na urafiki wao, akisema uhusiano wao ulivuka mipaka ya siasa.
Pia aliwashukuru wanachama wa Jubilee kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuwa katibu mkuu kwa miaka minne na naibu kiongozi wa chama…