WAKAZI wa maeneo mbalimbali ya Pwani wameingiwa na hofu kutokana na ongezeko la mashambulizi ya magenge yanayotumia mapanga, wizi wa pikipiki na uporaji, hasa nyakati za usiku.
Mjini Mombasa, waendesha bodaboda katika maeneo ya Kisauni na Likoni wanasema wahalifu huwarai hadi maeneo yaliyotengwa, kisha kuwashambulia na kuwaibia pikipiki, simu na vitu vingine vya thamani.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Vocal Africa limeonya kuwa maeneo ya Likoni na Kisauni yamekuwa hatari kutokana na mashambulizi yanayotokea hata mchana.
Shirika hilo limehusisha hali hiyo na ukosefu wa taa za barabarani na kamera za CCTV, likisema giza huwapa wahalifu nafasi ya kushambulia na kutoroka bila kutambuliwa.
Ndani ya wiki moja, angalau waendesha bodaboda wanane waliripotiwa kushambuliwa na kujeruhiwa Kisauni, hasa Mshomoroni, Barsheba na Bakarani.
Septemba 15, Said Faiz Khamis alishambuliwa na kundi la zaidi ya watu 10 waliokuwa na silaha eneo la Barsheba saa tano usiku.
Alijeruhiwa kichwani na vidoleni huku pikipiki yake ikipatikana baadaye katika kituo cha polisi cha Kiembeni.
Alisema awali alikuwa ameibiwa pikipiki nyingine na simu karibu na Kongowea. Siku iliyofuata, mwendesha bodaboda Chai Chivatsi alishambuliwa Bakarani na kujeruhiwa vidole, huku pikipiki yake ikiibwa.
Hali hiyo imewalazimu baadhi ya waendesha bodaboda kusita kufanya kazi usiku, wakihofia kupoteza maisha na mali yao.
Wakazi pia wamelalamikia wahalifu wanaotumia tuk-tuk kuwavizia abiria.