Chuo Kikuu cha Rongo kilipokuwa kikifanya mahafali yake ya 11 mjini Migori Ijumaa, aliyekuwa gavana wa kwanza wa kaunti hiyo, Okoth Obado, alikuwa akihukumiwa kifungo cha miaka 25 gerezani kwa mauaji ya mwanafunzi wa zamani wa chuo hicho, Sharon Otieno.
Baada ya kuhudumu kwa miaka tisa akiwa na mamlaka makubwa kisiasa, Obado sasa anaanza maisha ya gerezani pamoja na aliyekuwa msaidizi wake Michael Oyamo na aliyekuwa karani wa serikali ya kaunti ya Migori, Caspal Obiero.
Obado na Oyamo walihukumiwa kifungo cha miaka 25 kila mmoja, huku Obiero akipewa miaka 18 kwa kuhusika katika njama ya kumuua Sharon, aliyekuwa na umri wa miaka 26.
Hukumu hiyo ilifunga rasmi kesi iliyokuwa ikifuatiliwa kwa karibu nchini kwa miaka minane.Usiku wa Septemba 3, 2018, Sharon, ambaye alikuwa na watoto watatu na ujauzito wa miezi saba, alitekwa nyara pamoja na mwandishi wa habari wa Nation Media Group, Barack Odour.
Odour aliweza kutoroka kwa kuruka kutoka kwenye gari lililokuwa likienda kasi. Sharon hakubahatika. Baadaye mwili wake ulipatikana ukiwa na majeraha saba ya visu tumboni. Alifariki pamoja na mtoto aliyekuwa tumboni mwake.
Mauaji hayo yalizua hasira kubwa nchini huku wananchi wakitaka haki itendeke.
Katika uamuzi wake wa Julai 23, Jaji Cecilia Githua alisema kuwa ingawa hakukuwa na mtu aliyeshuhudia washtakiwa wakimuua Sharon, ushahidi uliowasilishwa mahakamani uliunganisha matukio yote na kuonyesha jinsi mauaji yalivyopangwa.