Aliyekuwa Gavana wa Migori Okoth Obado aliingia katika chumba cha mahakama jijini Nairobi Ijumaa saa mbili na dakika arobaini na tano asubuhi akiwa amevalia suti ya buluu, shati jeupe, tai na viatu vyeusi vilivyong’arishwa.
Wafuasi wake waliokuwa wamemsubiri walimkaribisha kwa jina Sibuor (Simba). Aliwajibu kwa kuinua mikono yote miwili akiwa amefungwa pingu.
Lakini saa tano asubuhi, Jaji Cecilia Githua alipoanza kusoma hukumu, ukumbi ulitulia. Kwa takriban dakika 40, Obado alisikiliza bila kuonyesha hisia huku mahakama ikieleza nafasi yake katika mauaji ya mwanafunzi wa chuo kikuu Sharon Otieno.
Jaji alimweleza kuwa alikuwa mpangaji mkuu, mfadhili na mtekelezaji wa mpango wa kumuua Sharon, aliyekuwa na umri wa miaka 26 na ujauzito wa miezi saba.
Mahakama ilipohitimisha na kumhukumu miaka 25 jela, baadhi ya wafuasi wake walilia, huku wengine wakizungumza kwa lugha ya Dholuo wakionyesha kutoamini hukumu hiyo. Hata hivyo, baadhi walipiga makofi baada ya mawakili wake kutangaza kuwa watakata rufaa.
Obado, ambaye sasa yuko katika miaka ya sitini, anaweza kuwa na zaidi ya miaka 90 atakapomaliza kifungo chake mwaka 2051, iwapo hukumu haitabadilishwa.
Kwa siku 123 tangu apatikane na hatia, alikuwa amezuiliwa rumande akisubiri hukumu. Akiwa gerezani Kamiti, alikuwa akiruhusiwa kupokea wageni kwa muda maalumu na kuhudhuria ibada Jumamosi.
Sasa maisha yake yamebadilika rasmi. Yeye pamoja na washtakiwa wenzake Michael Oyamo, aliyekuwa msaidizi wake, na Caspal Ojang Obiero, aliyekuwa mfanyakazi wa Kaunti…