WAHALIFU wa mtandaoni waliovamia na kudukua tovuti ya eCitizen wameanza kusambaza taarifa za kibinafsi za Wakenya zaidi ya 32 milioni katika mtandao fiche wa Dark Web, hatua inayowaweka mamilioni ya watu katika hatari ya utapeli.
Taarifa zilizopatikana na ‘Taifa Leo’ zinaonyesha kuwa wadukuzi hao waliiba rekodi za Wakenya 32,128,394, zikiwemo nakala za pasipoti, picha za pasipoti, nambari za vitambulisho vya kitaifa na tarehe za kuzaliwa.
Pia waliiba nambari za usajili za Mamlaka ya Ushuru Kenya (KRA), alama za vidole na nambari za kidijitali za afya zinazotumiwa na wanachama wa Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).Baadhi ya vitambulisho vya kikazi vya maafisa wa serikali pia vimesambazwa, hali inayozua hofu kuwa taarifa hizo zinaweza kutumiwa kuomba mikopo kwa majina yao au kuwatapeli.
Kikundi cha wahalifu wa mtandaoni kinachojulikana kama ByteToBreach kimekiri kuhusika na shambulizi hilo.Kikundi hicho kinadai kuwa kiliingia katika mifumo ya eCitizen na kuiba gigabaiti 600 za stakabadhi za kuthibitisha utambulisho wa wateja, gigabaiti 100 za taarifa za data na gigabaiti 40 za msimbo unaoendesha mifumo hiyo.Taarifa hizo ziligunduliwa Jumatatu na kampuni ya Amerika ya usalama wa mtandao, Vecert, inayofuatilia vitisho na shughuli za wahalifu katika mitandao fiche.
Wachunguzi wa kampuni hiyo walikagua rekodi za wahalifu hao na kubaini kuwa huenda walipata nafasi ya kuingia katika mitambo ya eCitizen Novemba 15 kwa kutumia udhaifu katika data inayotumika kuthibitisha utambulisho wa watumiaji.Dark…