WAKENYA wanaomkosoa Rais William Ruto huenda wakasahau kuwa marais wanne waliomtangulia pia walikumbwa na tuhuma za ufisadi, mauaji ya kiholela, matumizi mabaya ya mamlaka na upendeleo wa kisiasa.
Tangu enzi za Rais wa kwanza Jomo Kenyatta hadi utawala wa Uhuru Kenyatta, masuala hayo yamekuwa sehemu ya historia ya uongozi wa Kenya.
Wakati wa utawala wa Jomo Kenyatta, suala la ardhi lilikuwa mojawapo ya changamoto kubwa. Wakosoaji wanasema rais huyo na watu wake wa karibu walitumia mamlaka ya serikali kujinyakulia maeneo makubwa ya ardhi katika Bonde la Ufa na Pwani.
Wapinzani wa serikali yake pia walikabiliwa na ukandamizaji, huku mauaji ya wanasiasa kama Pio Gama Pinto, Tom Mboya na JM Kariuki yakitia doa utawala wake.
Mrithi wake, Daniel arap Moi, aliongoza kwa miaka 24 iliyokumbukwa kwa ukandamizaji wa wapinzani. Mwaka 1982 alibadilisha Katiba na kufanya Kenya kuwa nchi ya mfumo wa chama kimoja, huku wakosoaji wakikamatwa na kuzuiliwa bila kufikishwa mahakamani.
Mauaji ya Wagalla mwaka 1984 na mauaji ambayo hayajatatuliwa ya Waziri wa Masuala ya Kigeni Robert Ouko mwaka 1990 yalizidisha wasiwasi kuhusu matumizi mabaya ya mamlaka.
Pia, kashfa ya Goldenberg ilitajwa kuwa mojawapo ya visa vikubwa vya ufisadi nchini.
Mwai Kibaki aliingia madarakani akiwa na matumaini ya mageuzi, lakini utawala wake pia ulikumbwa na changamoto. Kashfa ya Anglo-Leasing iliharibu sifa ya serikali yake katika muhula wa kwanza.