WAPO vipusa wanaovutiwa zaidi na wanaume wanaowapa wakati mgumu, huku wanaume wenye upendo, heshima na msimamo wakiachwa pembeni.
Lakini je, ni kweli mwanamke humkataa mwanaume mwema na baadaye kujuta?
Katika ulimwengu wa mapenzi, kuna swali ambalo limezua mijadala mingi: Je, vidosho wanapendelea wanaume wanaowatesa kihisia kuliko wale wanaowapa upendo wa kweli, heshima na usalama?
Hoja inayozua mjadala ni kwamba baadhi ya mademu huvutiwa zaidi na wanaume wanaowafanya wajitahidi kupata mapenzi yao, huku wakikosa kuvutiwa na wanaume wanaoonyesha nia ya dhati tangu mwanzo.
Kwa mtazamo huu, mwanaume mwaminifu, mwenye msimamo, anayejali na asiyecheza na hisia za mwanamke anaweza kuonekana kama mtu asiye na msisimko.
Kinyume chake, mwanaume ambaye ni mgumu kueleweka, anayepotea bila maelezo na kumfanya mwanamke apiganie nafasi katika maisha yake anaweza kuonekana kuwa na mvuto mkubwa.
Wanaounga mkono hoja hii wanasema kuwa baadhi ya watu huchanganya mapenzi yenye afya na kuchoshana, huku wakitafsiri mahusiano yenye migogoro na kutokuwa na uhakika kuwa yenye msisimko.
Hoja nyingine ni kwamba baadhi ya vipusa huvutiwa na wanaume wanaotamaniwa na wanawake wengine.
Mwanaume aliye kwenye uhusiano mwingine au anayehusishwa na wanawake wengi anaweza kuonekana kuwa na thamani kubwa kutokana na ushindani unaomzunguka.
Katika hali hiyo, mwanamke anaweza kujikuta akishindania upendo na uangalizi wa mwanaume ambaye hana nia ya kujitoa kikamilifu katika uhusiano mmoja.