TAMAA ya kuwania nyadhifa za kisiasa imeanza kutikisa serikali ya Rais William Ruto, huku mawaziri, makatibu wa wizara na maafisa wakuu wa Ikulu wakijiandaa kujiuzulu ili kushiriki uchaguzi mkuu wa Agosti 2027.
Miongoni mwa wanaotajwa ni Mdhibiti wa Ikulu Katoo Ole Metito, msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed na Mawaziri Lee Kinyanjui na Geoffrey Ruku.
Wengine ni mawaziri Alice Wahome na Alfred Mutua pamoja na mshauri wa Rais Charles Keter.
Makataa ya kisheria ya Februari 10, 2027, yanakaribia na huenda yakasababisha mabadiliko makubwa katika serikali, ikiwa maafisa hao wataamua kuondoka ili kujipigia debe kwa wapigakura.
Metito anamezea mate kiti cha ugavana Kajiado, ambako anatarajiwa kukabiliana na Gavana Joseph Ole Lenku, ambaye anahudumu muhula wake wa pili na wa mwisho.
Utafiti wa TIFA uliochapishwa Novemba 24 ulimweka Metito mbele kwa asilimia 59 dhidi ya Kanar Seki Lenku aliyepata asilimia 21.
Hata hivyo, matokeo hayo ni picha ya awali ya umaarufu wa wagombeaji.
Metito, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Kajiado Kusini na Waziri wa Usalama wa Ndani, alishindwa na Lenku katika uchaguzi wa 2022 kwa kura 111,725 dhidi ya 117,600.
Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed naye analenga ubunge Kamukunji. Chanzo kilicho karibu na Ikulu kimesema azma yake tayari imekubaliwa na Rais Ruto.
Mohamed amekuwa akishiriki shughuli za kijamii katika eneo hilo na amepata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa Kamukunji waliokutana…