RAIS William Ruto amewashambulia viongozi wa upinzani akiwalaumu kwa kujali maslahi yao binafsi badala ya masuala yanayowahusu Wakenya.
Akiwa katika ziara ya maendeleo kaunti za Busia na Bungoma jana, Rais alisema wapinzani wamekuwa wakitumia muda mwingi kuzozana kuhusu nani atawania urais mwaka 2027 badala ya kuandaa mipango ya maendeleo.
Alisema serikali yake inaendelea kutekeleza miradi huku wapinzani wakihangaika na siasa za urithi.
“Hawa wamekaa zaidi ya mwaka mmoja wakibishana kuhusu mgombea wao wa urais. Ikiwa hawawezi kukubaliana kuhusu mtu mmoja, watafikiriaje ajenda ya Wakenya wa kawaida?” akauliza.
Ruto alitetea rekodi ya serikali yake akisema imewekeza katika barabara, masoko, elimu na afya.
Alisema Sh21 bilioni zimetengwa kujenga kilomita 210 za barabara na Sh75 milioni kwa soko la kisasa la Misikhu.
Alisema serikali imefufua kiwanda cha sukari cha Nzoia na kwamba atatembelea Mumias Jumatatu kutoa bonasi kwa wakulima wa miwa.
Katika elimu, alisema serikali imeajiri walimu zaidi ya 100,000 na itawapa walioajiriwa na bodi za shule kazi za kudumu.
Pia alisema asilimia 55 ya wakazi wa Bungoma wamejiandikisha katika Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).
Rais alizindua ujenzi wa barabara ya Butula-Amukura yenye urefu wa kilomita 55.
Pia alizindua soko la kisasa la Bumala lililogharimu Sh230 milioni na linalotarajiwa kuwahudumia wafanyabiashara zaidi ya 300.
Alisema serikali itaunganisha familia 16,000 Busia na umeme kwa gharama ya Sh2 bilioni.