Vuguvugu la Linda Mwananchi linaloongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna limepiga hatua baada ya wajumbe wa chama cha The Equitable Party (TEP) kuidhinisha kibadilishwe jina, rangi, nembo na makao makuu ya chama hicho.
Hata hivyo, maswali kuhusu uhalali wa mabadiliko hayo na uwezo wa chama kukamilisha taratibu za kisheria kabla ya uchaguzi wa 2027 bado yanazua wasiwasi.
Katika mkutano wa kitaifa wa wajumbe (NDC), uliofanyika bila wanahabari, wajumbe waliidhinisha pia marekebisho ya katiba na kanuni za uteuzi wa wagombeaji, pamoja na mazungumzo ya kuunda miungano na vyama vingine vyenye misimamo inayofanana.
Hata hivyo, mkutano huo haukufanya uchaguzi wa viongozi wapya, baada ya chama kuhakikishia Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa kuwa hakungekuwa na uchaguzi Novemba 13.
Ahadi hiyo ilitolewa kufuatia kesi iliyowasilishwa na mwanachama James Onyango Nyangor, aliyepinga kufanyika kwa uchaguzi wakati wa mkutano huo.
Jopo liliruhusu mkutano kuendelea baada ya kutupilia mbali ombi la kuusimamisha. Iliacha malalamishi kuhusu uteuzi wa wajumbe na mabadiliko ya chama yasikilizwe kikamilifu, huku ikihifadhi mamlaka ya kubatilisha maamuzi yatakayopatikana kuwa yalifanywa kinyume cha sheria.
Wanachama Paul Kiragu Gachoka na Pamela Achieng Simwata walikuwa wamepinga mkutano huo, wakisema chama hakukuwa na baraza halali la uchaguzi la kuchagua wajumbe. Pia walidai Baraza la Kitaifa la Uongozi halikuwa limeidhinisha ajenda na chama hakikuwa na bodi ya uchaguzi iliyoundwa ipasavyo.

