Baada ya miezi kadhaa ya juhudi za kuwapatanisha, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua wameanza kuonyesha dalili za kurejesha uhusiano wao wa kisiasa, hatua inayoweza kubadilisha mipango ya upinzani kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.
Hii pia inaweza kuathiri kampeni za Rais William Ruto kudumisha uungwaji mkono katika eneo la Mlima Kenya hasa baada ya kutofautiana na Bw Gachagua.
Kufufua uhusiano wao kunaibua maswali kuhusu nani atakuwa msemaji mkuu wa kisiasa wa eneo la Mlima Kenya, huku Uhuru akiwa na ushawishi na mitandao aliyojenga akihudumu kama rais kwa miaka 10, na Gachagua akijitahidi kujijenga kama kiongozi mpya wa kisiasa wa eneo hilo.
Baadhi ya wachambuzi wanasema Gachagua anahitaji ushirikiano huo ili kuimarisha mamlaka yake ya kisiasa, huku wengine wakionya kuwa anaweza kupoteza nafasi yake ndani ya upinzani iwapo Uhuru atakuwa kitovu cha mazungumzo ya kisiasa.
Mhadhiri wa chuo kikuu na mchambuzi wa siasa Profesa Macharia Munene anasema kurejea kwa maelewano kati ya viongozi hao kunaweza kuwa na manufaa kwao na kwa eneo hilo, lakini swali kubwa litakuwa namna ya kumpata mgombea mmoja wa urais wa upinzani.
“Uhuru si mgombeaji katika uchaguzi huu. Gachagua pia huenda asiwe mgombeaji wa upinzani. Swali ni jinsi watakavyokubaliana kuhusu mgombea wa urais wa upinzani kushindana na Rais Ruto,” alisema.