KAKA ya aliyekuwa makamu wa rais marehemu George Saitoti, ameunga mkono madai ya James Njage anayetaka kutambuliwa kama mwana wa mwanasiasa huyo aliyehudumu kama mbunge wa Kajiado kaskazini na kupewa sehemu ya urithi wake.
Bw Ronald Musengi, aliyekuwa kamishna wa Tume ya Huduma za Polisi, alisema vipimo vya DNA alivyofanyiwa pamoja na Bw Njage vimethibitisha kuwa ni mpwa wake wa damu.
Katika ripoti iliyowasilishwa mahakamani, uwezekano wa wawili hao kuwa na uhusiano wa damu ulionyeshwa kuwa asilimia 99.9999.
Bw Musengi alisema aliamua kufanyiwa vipimo hivyo baada ya kukutana na Bw Njage na kusikiliza simulizi yake kuhusu maisha yake ya utotoni na uhusiano wake na marehemu Saitoti.
Alisema maelezo ya Bw Njage kuhusu siku aliyofariki baba yake yalimfanya atake kuthibitisha uhusiano wao.
Bw Njage anataka mahakama kufungua upya kesi ya urithi wa Saitoti, akisema aliachwa nje wakati mali ya marehemu ilipogawanywa kati ya mjane wake Margaret Wanjiku Saitoti na mwanawe Zachary Musengi.
Anasema wakati mali hiyo ilipogawanywa alikuwa mtoto mdogo akiishi nje ya Kenya, hivyo hakufahamishwa kuhusu kesi wala kupewa nafasi ya kudai haki yake.
Pia anataka wasimamizi wa mirathi kutoa hesabu kamili ya mali, mapato ya nyumba za kukodisha, uwekezaji, miamala ya benki na madeni.
Bw Njage pia ameiomba mahakama kuruhusu mwili wa Saitoti kufukuliwa ili vipimo vingine vya DNA vifanywe na wataalamu wa serikali na maabara binafsi.