CHUO Kikuu cha Moi, ambacho kinakabiliwa na changamoto kubwa kifedha, kimeanzisha kilimo cha miwa kwa kiwango kikubwa kama njia ya kujiongezea mapato na kupunguza kutegemea fedha za serikali.
Chuo hicho tayari kimepanda miwa katika ekari 750 na kina mipango ya kuongeza eneo hilo hadi ekari 1,500.
Mradi huo unaogharimu Sh105 milioni, unalenga kugeuza ardhi kubwa ya chuo kuwa chanzo cha mapato, kusaidia shughuli za masomo na kutoa ajira kwa wakazi wa maeneo jirani.
Naibu Chansela wa Chuo hicho Profesa Kiplagat Kotut, alisema wameamua kutumia rasilimali ya ardhi waliyonayo kujipatia mapato badala ya kutegemea mgao wa serikali pekee.
[caption id="attachment_194032" align="alignnone" width="2000"] Chuo Kikuu cha Moi. Picha|Maktaba[/caption] “Lengo letu kuu ni kuhakikisha chuo kinaendesha shughuli zake bila matatizo. Ili kufanikisha hilo, ni lazima tujipatie fedha za kutosha kupitia miradi yetu,” alisema Profesa Kotut.
Alisema chuo kina takriban ekari 3,000 na kinapanga kutumia karibu nusu yake kulima miwa ili kukabiliana na changamoto za kifedha, huku kikisaidia pia masomo ya kilimo na uhandisi.
Akizungumza Jumanne alipokagua maendeleo ya shamba hilo, alisema mradi huo ulianzishwa baada ya mashauriano na kampuni za kusaga miwa, wadau wa kilimo na wakazi wa eneo hilo.
Chuo hicho kinashirikiana na West Kenya Sugar Company, ambayo inatoa utaalamu na ushauri kuhusu utunzaji wa mimea. Kampuni hiyo pia itanunua miwa itakapokomaa na kuisaga.